🌿 SOMO LA LEO: “KUANZA UPYA NA MUNGU”
📖 Mstari mkuu — 2 Wakorintho 5:17
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.”
Mafundisho:
Mungu hakuiti uendelee kuishi chini ya makosa ya jana. Ukiamua kumkaribia, kuna nafasi ya kuanza ukurasa mpya. Mwanzo mpya hauimaanishi kwamba maisha yatakuwa bila changamoto; maana yake ni kwamba hutakabiliana nazo ukiwa mtu yuleyule wa zamani.
📖 1. Isaya 43:18–19 — Mungu anaenda kufanya jambo jipya
Mungu anasema tusishikilie mambo ya zamani kwa namna inayotuzuia kuona kile anachotaka kufanya.
Jifunze:
- Acha kujihukumu kwa makosa yaliyopita.
- Usiruhusu kushindwa kwa jana kuamua kesho yako.
- Mpe Mungu nafasi ya kuanza kazi mpya ndani yako.
Swali la kujiuliza:
Ni jambo gani la zamani ambalo ninahitaji kumkabidhi Mungu leo?
📖 2. Yakobo 4:8 — Kuwa karibu na Mungu
“Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.”
Huu ni mstari muhimu sana kwa mtu anayetaka kuwa karibu na Mungu.
Kumkaribia Mungu kunahitaji hatua zifuatazo:
- Kuomba kila siku.
- Kusoma Neno lake kila siku.
- Kutubu kwa moyo wa kweli.
- Kuacha mambo yanayotutenga naye.
- Kujifunza kumtegemea katika maamuzi yetu.
Usisubiri mpaka ujisikie “mkamilifu” ndipo umkaribie Mungu. Mkaribie Mungu ukiwa ulivyo, naye aanze kukubadilisha.
📖 3. Zaburi 51:10 — Omba moyo mpya
“Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.”
Hili ni ombi zuri sana kwa mtu anayeanza upya.
Badala ya kusema tu, “Mungu nibariki,” pia sema:
“Mungu nibadilishe.”
Kwa sababu wakati mwingine tunahitaji si mazingira mapya tu, bali moyo mpya, mtazamo mpya na tabia mpya.
📖 4. Warumi 12:2 — Badilika kwa kufanya mambo mapya kwa nia
Usikubali kila kitu kinachokuzunguka kikufanye uwe mtu yuleyule.
Mungu anataka kubadilisha namna tunavyofikiri, tunavyoamua na tunavyoishi.
Leo jiulize:
- Mawazo yangu yananisogeza kwa Mungu au mbali naye?
- Marafiki zangu wananijenga au kunivunja?
- Ninachotazama na kusikiliza kinanisaidia kuwa mtu ninayetaka kuwa?
- Maamuzi yangu yanaonyesha mtu mpya ninayetaka kuwa?
📖 5. Wafilipi 3:13–14 — Songa mbele usikatishwe tamaa.
Paulo anatufundisha kutokufungwa na yaliyopita, bali kuendelea kuelekea mbele.
Usiruhusu:
- kosa lako la jana,
- kushindwa kwako,
- watu waliokuumiza na kukuzungukuka,
- Maisha yako ya zamani na watu wako wa karibu wasikurudishe nyuma.
🔥 FUNZO KUU LA LEO
Kuwa mtu mpya na kuwa na Mungu si tukio la siku moja tu; ni safari ya kila siku.
Anza na mambo haya matano:
1. Dakika 10–15 za maombi kila siku.
Mwambie Mungu kwa uaminifu kile kilicho moyoni mwako.
2. Soma Biblia kila siku.
Anza na kitabu cha Injili ya Yohana kama unataka kumjua Yesu kwa undani zaidi.
3. Tubu bila kujitetea.
Ukikosea, rudi kwa Mungu tubu badala ya kukimbia na kuleta excuses.
4. Ondoa kinachokurudisha kwenye maisha ya zamani.
Baadhi ya mazingira, tabia au mahusiano yanaweza kufanya safari yako kuwa ngumu.
5. Jenga tabia ya kumtafuta Mungu hata unapokuwa na furaha.
Usimtafute Mungu wakati wa matatizo tu. Mtafute pia wakati mambo yako yanaenda vizuri.
🙏 MAOMBI YA LEO.
“Ee Mungu wangu, leo ninakuja mbele zako nikitamani kuwa mtu mpya. Nisamehe pale nilipokosea na kunitenga na mapenzi yako. Niumbie moyo safi na uifanye upya roho yangu. Nisaidie kuacha yale yanayonirudisha nyuma na kunipa nguvu ya kuishi maisha yanayokupendeza. Nipe kiu ya kusoma Neno lako, kupenda maombi na kutembea karibu nawe. Niongoze katika maamuzi yangu, mahusiano yangu na maisha yangu yote. Kuanzia leo, nataka kukujua zaidi na kukutegemea zaidi. Katika jina la Yesu, Amina.”
🌅 Kauli ya kujikumbusha leo
“Yaliyopita hayataamua maisha yangu. Kwa msaada wa Mungu, ninaweza kuanza upya, kubadilika, na kukua katika uhusiano wangu na Mungu.”


0 Comments